Friday, January 25, 2013

T unawatakia kwa pamoja heri katika utumishi kwenye shamba la Bwana, viongozi wote wapya.

Mwenyekiti wa Thisdaso Mzumbe(kulia) ndg. Mujaya Mujaya, kulia ni Upendo Mlengu Kaimu Mwenyekiti wa Thisdaso Mzumbe.

Monday, December 17, 2012

Je, sabato ilianzia kwa Wayahudi? Je, ni ya wayahudi tu?



    Watu wengi wanajiuliza kuwa sabato ilianza kwa wayahudi? Na kama ni hivyo basi sisi hatupaswi kutunza na kuishika maana niya wayahudi. Katika hili tutaiuliza Biblia yenyewe itupatie majibu, au siyo?
Biblia inatwambia Sabato ilianzishwa katika Bustani ya Edeni siku ya SABA baada ya uumbaji. Mwanzo.2:1-3, “Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. NA SIKU YA SABA Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; AKASTAREHE SIKU YA SABA, AKAACHA KUFANYA KAZI YAKE YOTE ALIYOIFANYA, Mungu akaibariki siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, AKAACHA KUFANYA KAZI yake yote aliyoiumba na kuifanya.” Hapa tunaona kuwa sabato ya kwanza kabisa katika historia ilikuwa tarehe 07-01-01 au mwaka 4000K.K. Katika sabato hii, kulikuwa na WATU WAWILI TU Adamu na Hawa ambao hawakuwa wayahudi sawa? Unajua kama Adamu na Hawa wangekua wayahudi basi watu wote tungekuwa wayahudi maana hawa walikuwa wazazi wetu wa kwanza ambamo watu wote tumetokea kwao.
Ibrahimu aliishi miaka 2000 kabla ya kuanzishwa kwa taifa la Uyahudi, kabla ya kipindi cha Musa cha kutoka Misri kwenda Kanani. Lakini biblia inamshuudia kuwa aliishika Sabato maana alishika amri na sheria za Mungu hata kabla hazijatolewa katika mlima Sinai kwa wana wa Israeli. Mwanzo. 26:5, inasema “Kwa sababu Ibrahimu alisikia sauti yangu, akayahifadhi maagizo yangu, na AMRI zangu, na hukumu zangu, na SHERIA zangu.” Hivyo Ibrahimu alishika amri za Mungu zote ikiwemo na sabato tazama Kutoka. 21:8-11, na zingatia pia Ibrahimu alishika amri zote za Mungu maana kama angevunja moja agekua hajazishika. Tazama Yakobo2:10 na Mathayo5:17-19. Pia wana wa Israeli walishika sabato hata kabla hawajapewa amri za Mungu katika mlima Sinai hili tunaliona katika Kutoka.16:23-27. Ndio maana wakati Mungu anatoa Amri zake kwa Israeli anasema “IKUMBUKE SIKU YA SABATO UITAKASE siku sita ufanye kazi utende mambo yako yote….” Kutoka.20:8 aliwambia waikumbuke maana walikuwa wanaijua. Katika utumwa wa Misri wana wa Israeli walikuwa wamesahau sabato ya BWANA na kama wangekua hawaijui asimgewambia waikumbuke.
Yesu alipokuja alisema sabato ilifanyika kwajili ya watu wote, Yesu “akawaambia, sabato ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya sabato.” Marko.2:27 Hivyo tunaona kuwa sabato ilifanyika kwa ajili ya MWANADAMU, ndugu je wewe nawe ni mwanadamu? Kama ndiyo basi mshukuru sana Mungu maana ameumba Sabato siku ya SABA kwa ajili yako uifurahie kwa pumziko takatifu.
Baada ya Yesu kwenda mbinguni, mitume waliendelea kushika Sabato pamoja na mataifa mengine wasiokuwa Wayahudi. Katika matendo.13:42,44 tunaona mkutano uliofanyika siku ya sabato ambao mataifa walimsihi Paulo arudie hubiri lake la sabato katika sabato inayofata: ZINGATIA ‘Kama wangekuwa wanasali Jumapili, wale watu wangesema wakutane kesho yake lakini haikuwa ivyo maana walisema Sabato ijayo. Na sabato iliyofata walikuja mji mzimakusikiliza hubiri la Paulo’ adi wayahudi waliokuwa wapinzani wa kazi ya Mungu wakaanza kumwonea wivu. Tazama pia Matendo.18:4, Paulo “akatoa hoja zake katika sinagogi(kanisa) KILA SABATO akajaribu kuwavuta Wayahudi na Wayunani.”
Biblia haisemi sehemu yoyote kuwa sabato ni ya wayahudi tu, hii kusema watu wengine wasio wayahudi hawatakiwi kushika sabato ya  siku ya saba j/mosi. Madai haya hayana ukweli maana kuvunja sabato kunamfanya mtu awe mvunja sheria zote za Mungu kwani ukuvunja moja umevunja zote.
Karibu sana katika raha ya sabato maana ni raha pekee kwa watu wa Mungu, Waebrania.4:9 inasema “basi imesalia raha ya sabato kwa watu wa Mungu.”
 Imeandaliwa na muinjilisti MUJAYA M.J
 

Habari wapendwa na ndugu katika Kristo? nawasalimu kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo.
Napenda kuwashukuru sana THISDASO MZUMBE na MARAFIKI zetu kwa kujitoa kwenu katika kufanikisha kazi ya Mungu kwa mioyo na zaidi kwa michango yenu mhimu sana. Sasa baada ya kutoka katika Effort na sabato ya wageni, Mungu anatuongoza katika Video recording ya kwaya yetu na Effort Kubwa sana kipindi cha likizo ya February. Hivyo natumia tena nafasi hii kuwasihi kutoa michango yenu kama ambavyo Roho wa Mungu amekuwa akiwaongoza ili kuendeleza kazi yake.
Upatapo habari hii, tafadhali shiriki baraka za Mungu kwa kumwambia na mwenzako.
BWANA akubariki sana.
Mujaya MJ, Mwenyekiti wa tawi.

Saturday, November 17, 2012

MWALIMU MWENYE UKWELI HALISI


WASIFU WA MWALIMU

        Tangazo la biashara: Ahadi kwamba atapunguza kilo 11 katika majuma mawili kwa kutumia kitu kilichokuwa kinatangazwa.
       Chumvi nyingi ilikuwa imeongezwa: alipunguza siyo zaidi ya nusu kilo.
        Watabiri wa hali ya hewa walitangaza kuwa kesho yake ingekuwa siku ya jua na joto mwisho wa mwezi wa nne (Aprili).
       Pilipili ilikuwa imeongezwa: kesho yake kukawa na mawingu, radi na mvua kubwa ya mawe.
        Yule jamaa aliyekuja kukuuzia ile simu pale kwenye stendi ya basi; alikuuzia kwa nusu ya bei halisi ya ile simu.
       Huyu alikuwa amechanganya chumvi na pilipili na chloroquine: Alikuwa ameiiba simu hiyo kwa abiria mwingine kama wewe muda mfupi kabla. 
              
Hivyo ndivyo sifa za watu zinavyotangazwa na kuwekwa mbele za jamii ya wakazi wa dunia. Kuna chumvi nyingi, pilipili na hata sumu zinazochanganywa ndani yake. Ukweli wenyewe hauelezwi, na uongo mwingi hutangulizwa!
        Wengi wanasemwa katika hali ambayo si ya kweli (too good to be true)! Na bado ulimwengu unanunua taarifa hizo na kuzishangilia.
        Mwalimu wa kweli hatangazwi na kile watu wasemacho kumhusu, bali kwa yale aliyoyatenda, anayoyatenda na atakayotatenda! Wasifu wake unajiuza; “chema chajiuza, kibaya chajitembeza”
        Mwalimu Mwenye Ukweli Halisi anajiuza kwa kazi zake za thamani kuu!!!

WASIFU WA MWALIMU
        JE, YEYE ALIKUWA NANI?
        YEYE NI NANI?
        ALIFANYA NINI?
        ANAFANYA NINI?
        ATAFANYA NINI?
        WASIFU WAKE UNAKUHUSUJE?

        YEYE ALIKUWA NANI NA NI NANI SASA?
      Yohana 1:1-3, 14 “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika….     Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”
        1 Yohana 5:8: “Kwa maana wako watatu washuhudiao mbinguni, Baba, na Neno, na Roho Mtakatifu, na watatu hawa ni umoja.”

        ALIKUWAKO KWA MUNGU, NAYE ALIKUWA MUNGU:
         Yohana 8:58 “Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko.”
        Waebrania 1:1,2 Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu.
        Mwanzo 1:26  “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu…”
         Kumbukumbu la Torati 6:4 “Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja.”
         Yohana 10:30 “Mimi na Baba tu umoja.” 

        CHEO “MWANA” KILIANZIA WAPI?



Sunday, September 9, 2012

FAHAMU SEHEMU TULIYOPO KATIKA HISTORIA, NA MAMBO YATAKAYOTOKEA HIVI KARIBUNI.


“Je, wajua tupo wapi katika historia na tunaelekea wapi?”
“Heri asomaye na wao wayasikiao maneno ya unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati u karibu. Ufunuo. 1:3

Ni nini unachoamini sana? Ambapo umeweka matumaini na mategemeo yako yote? Kama ukialikwa leo kuonana na mtu mhimu sana utafanya nini? Huenda ukachagua nguo nzuri unayoiamini sana. Kumwamini MUNGU ni jambo la msingi kwa kila mtu. Je, tunamwamini MUNGU kwa kiwango gani? Tatizo letu kubwa wanadamu hatumwamini Mungu kwa asilimia zote, mara nyingi MUNGU si tegemeo na kimbilio wakati wote, tunaona MUNGU anaweza baadhi ya mambo fulani tu na mengine hawezi. Pia watu wengi humwabudu MUNGU na wengine humtumikia lakini cha ajabu hawamwamini.
Mungu anatwambia mambo kabla hayajatokea ili yatakapotokea tumwamini, Yesu anasema katika Yohana. 13:19, “Tangu sasa nawaambia kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini ya kuwa mimi ndiye.” Hivyo Mungu anatangaza mambo ya siku za usoni kabla hayajatukia ili tuyaonapo yakitimia tumwamini, Yohana. 14:29 inaongeza “Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini.” Hebu tazama Mika anatoa unabii wa kuzaliwa Yesu katika bethlehemu, Mika. 5:2 “Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliyemdogo kuwa miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala wa Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.” Jambo hili likatimia miaka mingi baadaye kama unabii ulivyosema, Mathayo. 2:1 inasema “Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode… kisha mfalme Herode akawaita wakuu wa makuhani wote na waandishi kuwauliza Kristo azaliwa wapi? Ndipo alipojibiwa, Mathayo. 2:5 “Nao wakamwambia, Katika Bethlehemu ya Uyahudi: maana ndivyo ilivyoandikwa na nabii.” Hivyo Yesu alizaliwa kama ilivyatabiriwa na nabii Mika.
Jambo hili linathibitisha imani yetu kuwa Mungu ni mkuu, na linatupatia sababu ya kumwamini MUNGU wa mbinguni.
Unabii ni taa inayotuangaza, biblia inasema katika 2 Petro. 1:19, “Nasi tuna lile neno la unabii lililo imara zaidi, ambalo, mkiliangalia kama taa ing’aayo katika giza, mwafanya vyema, mpaka kutakapopambazuka, na nyota ya asubuhi kuzuka mioyoni mwenu.” Ili tusiwe katika giza, Mungu hutupatia unabii kwa kuwafunulia manabii siri yake, imeandikwa katika Amosi. 3:7 kuwa, “Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lolote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.” Na unabii ni imara zaidi maana hutimia sawasawa na ulivyotabiliwa nasi tunapouangalia unabii biblia inasema tunafanya vema kwani hatutakuwa gizani.
Pia kabla hatujauangalia unabii lazima tujue neno hili kwanza kwamba, unabii unatakiwa utafsiriwe si kama apendavyo mtu fulani, 2 Petro.1:20-21; 1 Wakorintho. 1:13,
Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii hukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, waliongozwa na Roho Mtakatifu”. “Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni”
Unabii unapaswa kutafsiriwa kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu maana kwa kupitia Yeye(Roho Mtakatifu) ulitolewa kwa watumishi wa Mungu manabii, na kwakuwa ni mambo ya rohoni lazima yatafsiriwe kwa maneno ya rohoni. Yesu alizungumza habari za kuja Roho Mtakatifu kwa kusema, Yohana. 16:13 “Lakini atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena na mambo yajayo atawapasha habari zake.” Hapa tunaona kuwa Roho Mtakatifu ni (a) kiongozi katika kweli yote (b) ananena yote vilevile kama alivyoyasikia toka kwa Baba na (c) atapasha habari za mambo yajayo. 1 Wakorintho. 2:10, inasema pia “Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.” Sababu hizi pekee zinatuonesha kuwa, Roho Mtakatifu pekee ndiye aletaye unabii kwa manabii hivyo yeye peke yake ndiye anayetoa tafsiri yake.
Mungu ndiye anayetoa unabii na unapofikia utimilifu wa wakati jambo hilo linatokea kama lilivyotabiriwa. Pia BWANA ana uwezo wa kuona mambo ambayo wanadamu watafanya siku za usoni, hivyo hutoa wakati kamili ambapo mambo hayo yatadhihilika, na muda huo unapofika unabii unatimia. Haiwezekani unabii wa uwongo utimie kwa wakati sahihi.
Unabii huthibitika tunapoangalia historia, maana Mungu ambaye aliona mambo yatakayofanywa na wanadamu, alitoa unabii juu yao, na wanadamu wanapoingia katika utendaji na kutenda kama yalivyotabiriwa, wanahistoria wananakili mambo ya wanadamu ambayo sasa yakifananishwa na unabii yanafanana kabisa.
Na sasa mambo yote yaliyopita katika historia na tunayoona yanaendelea kutendeka yapo katika unabii usiokosewa. Unaweza kujua wapi ulipotoka, wapi ulipo na wapi unapokwenda kwa kuutazama unabii wa biblia jinsi ulivyo na unavyodhihilika kabisa kwa uhakika katika historia. Unabii hutuwezesha kujua matukio ambayo yatatokea mbeleni na kuthibitisha imani yetu kwa Mungu pamoja na kuongeza imani yetu kwa MUNGU aliyeona mambo hayo yakitendeka; na kwa kupitia Roho wake akawavuvia manabii wakaandika katika vyuo(vitabu). Pia kutimia kwa unabii, utupatia uthibitisho wa ukweli wa NENO la Mungu ambamo umeandikwa.
Shetani hapendi kabisa watu wachunguze unabii, maana watajua hatma ya yale anayowaongoza kutenda na hivyo watamkataa na watamkimbia. Shetani huwafanya wajione wametingwa na kazi, huwapatia uchovu au hata usingizi na pengine kuweka jambo au kitu chochote ambacho kitatoa usikivu wao kwa neno la Mungu ili waokolewe. Wengine waliopata fursa ya kuujua unabii na kuona ukithibitika wazi katika historia, shetani anawaongoza wapuuzie ile neema ya Yesu iokowayo na maonyo waliyopata kutoka katika unabii. Haitatosha kujua unabii tu, kama hautaongeza uhusiano wako na MUNGU, na kukusogeza hadi kwenye msalaba wa Yesu ili uungame dhambi zote na kutokuamini, kutubu kwa dhati ili uhesabiwe haki kwa imani. Biblia inasema katika, Ufunuo. 1:3 “Heri asomaye na wao wayasikiao maneno ya unabii huu, na kuyashika yaliyoandikwa humo; kwa maana wakati u karibu.Hivyo heri si kwa anayeishia kusoma na kusikia unabii tu, bali kwa Yule anayeyashika yaliyoandikwa katika unabii. Tuna heri ndugu mpendwa kama tutatenga muda kusoma, kusikiliza na kushika maneno ya unabii.

NDOTO YA KIHISTORIA
Ilikuwa mwaka 604k.k, usiku mmoja katika jiji la Babeli, mfalme mashuhuri aliyetawala Dunia yote aliota ndoto ya maana sana na ilikuwa ya kihistoria. Ndoto hii ni yakihistoria maana historia yote ya ulimwengu tangu zamani za mfalme huyu Nebukadneza hadi mwisho wa dunia ilifunuliwa na MUNGU kwa mfalme Nebukadneza kwa njia ya ndoto. Kwa jinsi ndoto ilivyokuwa mfalme ilikatishwa usingizi wake na akafadhaika sana maana alitaka ajue tafsiri yake, ila baada ya kuota ndoto hiyo akaisahau.
Mfalme akatoa amri kuwaita waganga, na wachawi, na wahasiri, na wakaldayo ili kwanza wamweleze aliota nini, kisha wamwelezee tafsiri ya ndoto hiyo. Mfalme Nebukadneza aliamini kwamba miungu ya babeli, wenye hekima wake, waganga, wachawi, walozi na wasomi wa babeli wangempatia ndoto aliyoota na tafsiri ya ndoto hiyo. Je, wewe unapopata shida yoyote ni nani wa kwanza kumweleza? Pengine unaweza ukapeleka kwa msomi mashuhuri, wataalamu wa ushauri, wanasaikolojia, waganga wa jadi, wachawi, wasafisha nyota, watabiri, wachungaji na manabii wa uwongo, au rafiki yako mpendwa, mlezi, mpenzi au hata watu wenye hekima kama alivyofanya mfalme Nebukadneza. Lakini leo nakupa shauri umweleze Yesu kwanza, maana yeye anajishughulisha sana na mambo yetu, 1 Petro. 5:7, “huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.”  Lakini mfalme hakumtwika Mungu fadhaa zake bali wanadamu. Isaya nabii anaongeza, Isaya. 9:6 “Naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani.”
Mfalme alimwuliza shetani ndoto aliyoota pamoja na tafsiri yake, shetani aliyemletea fadhaa, woga na kukata tamaa angewezaje kumpatia pumziko mfalme Nebukadneza? Mara nyingi hata sisi tunakosa pumziko na ufumbuzi wa shida zetu maana tunampelekea adui yetu aliye msababishi wake azitatue kwajili yetu. Kwa kuwadanganya wazazi wetu wa kwanza katika Edeni shetani amesababisha matatizo na shida zote tuzionazo na zinazotupatazo leo, vita, njaa, magonjwa, chuki, ukame, ubinafsi, kukataliwa na vifo. Shetani anatuongoza kutenda dhambi huku akiwa ameficha matokeo mabaya ya dhambi yasionekane.
Biblia inasisitiza sana kwamba tusiwaendee waganga, wachawi, watabiri, wanajimu, wasafisha nyota n.k maana kwao hakuna asubuhi. Isaya. 8:19,20 inasema “Na wakati watakapokwambia, tafuta habari kwa watu wenye pepo na kwa wachawi; waliao kama ndege na kunong’ona; je Haiwapasi watu kutafuta habari kwa Mungu wao? Je, Waende kwa waliokufa kwa ajili ya watu walio hai?” Kipimocha kumpima ni lazima aenende kwa sheria na ushuhuda tu, biblia inaongeza, “na waende kwa sheria na ushuhuda; ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi.”
Kipindi fulani katika nchi ya Tanzania alizuka Babu, Loliondo Arusha aliyekuwa mchungaji mstaafu wa kanisa fulani la kikristo duniani, akashuhudia ya kwamba amepata mafunuo juu ya dawa ambayo inatibu magonjwa yote sugu ikiwemo ukimwi na akaambiwa dawa hiyo auze kwa pesa ya kitanzania sh. 500/= tu. Siku chache tu baada ya tangazo lake mamia, kisha maelfu ya watu toka sehemu mbalimbali  ndani na nje ya Tanzania walionekana wakienda loliondo kupata tiba ya kikombe. Watu wa kila hali walikwenda. Mtu mmoja aliyetamani sana kwenda kupata tiba ya kikombe aliniuliza ili apate msimamo wa neno la Mungu kuhusu tiba hiyo, nami nikamjibu (1) Lazima aenende kwa sheria na ushuhuda[1]  jambo ambalo hakuwa nalo. (2) aendane na manabii waliotangulia[2] jambo ambalo hakuwa nalo pia, hivyo nikamsihi sana asiende maana Mungu hatakuwa naye Loliondo. Biblia inasema jambo la mhimu sana hapa katika Kumbukumbu. 13:1-3,
“Kukizuka katikati yako nabii, au mwotaji wa ndoto, akikutolea ishara au ajabu, ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo; wewe usiyasikilize maneno ya nabii Yule, au Yule mwotaji wa ndoto, kwakuwa BWANA, Mungu wenu, yuawajaribu, apate kujua ya kwamba mwampenda BWANA, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote.”
Neno la MUNGU lipowazi sana hapa, kukizuka katikati yako nabii au mwotaji wa ndoto_babu alizuka kama nabii na mwotaji ndoto; akikutolea ishara au ajabu_babu alitoa ishara na ajabu kwa tiba yake; ikatukia ishara au hiyo ajabu_baadhi ya ishara na maajabu ya babu yalitimia na Neno linahitimisha kuwa USIYASIKILIZE MANENO YA NABII YULE, AU YULE MWOTAJI  WA NDOTO. Hilo ndilo neno la Mungu lisemavyo na hivi karibuni imethibitika kuwa dawa ile haikuponya magonjwa ya watu pia baadhi yao walifariki dunia kwa sababu mbalimbali.
Nebukadneza naye hakutaka kumpelekea Yesu fadhaa zake bali aliamua kuwapelekea watu aliowaamini kuwa wangempatia ndoto aliyoiota na tafsiri yake pia aliamini miungu ya babeli ingefanya hivyo. Lakini wote aliowategemea walishindwa, wakamwabia mfalme,  Danieli. 2:11 “Ni neno la ajabu, hili analolitaka mfalme, wala hapana mwingine awezaye kumwonyesha mfalme neno hilo,ila miungu, wasio na kikao na wenye mwili” hapa tunaona wakikili wazi kuwa hawawezi, pengine mfalme angewambia ndoto yake wangekuwa na la kumdanganya na ingekuwa vigumu kwao kusema ndoto aliyoiota mtu mwingine.
NDOTO YAWEKWA WAZI KWA MFALME
Tunaona katika habari hii, Mungu akimtumia mtumishi wake Danieli kumfunulia mfalme Nebukadneza ndoto aliyoiota pamoja na tafsiri yake. Danieli alikuwa mtumwa tu katika nchi ya babeli, alichukuliwa kama asiye starabika, ingawa Danieli pamoja na wenzake watatu yaani Shadraki, Meshaki na Abednego walionekana kuwa bora mara kumi zaidi kwenye mtihani wao wa mwisho wa chuo Danieli. 1:19-20 “Naye mfalme akazungumza nao; na miongoni mwao wote hawakuonekana waliokuwa kama Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria; kwaiyo wakasimama mbele ya mfalme. Na katika kila jambo la hekima na ufahamu aliowauliza mfalme, akawaona kuwa walifaa mara kumi zaidi ya waganga na wachawi waliokuwa katika ufalme wake.”, bado mfalme hakuona hitaji la kuwashirikisha katika kutoa ndoto aliyoiota pamoja na kumpatia mfalme tafsiri ya ndoto hiyo.
Kitendo cha Israeli kuwa mateka wa babeli, Mungu wa Israeli alionekana kama hana nguvu, kama si kitu ukilinganisha na miungu ya babeli. Na hapa kwa mfalme huyu mpagani, Mungu wa Israeli alitaka kudhihirisha nguvu na uwezo wake kupitia watu wake wanyenyekevu na dhaifu waliojitoa kwake. Maana biblia inasema katika 1 Wakorintho. 1:27, 28 “bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko;”
Ili kupata mafunuo ya ndoto ya mfalme pamoja na tafsiri yake, Danieli alishirikiana na wenzake katika kumwomba MUNGU wafunuliwe siri ile, Danieli. 2:17,18. Ndipo Danieli alifunuliwa siri hiyo ya ndoto ya mfalme katika njozi ya usiku. Biblia inasema “basi Danieli akamhimidi Mungu wa mbinguni.” Danieli. 2:19. Ili wasiaibike, Danieli na wenzake walikimbilia kwa Mungu, Zaburi. 46:1 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.” kama Daudi alivyosema katika Zaburi. 31:1, “Nimekukimbilia Wewe, BWANA, Nisiaibike milele. Kwa haki yako uniponye,” hili ndilo lilikuwa kimbilio lao, na MUNGU aliwajibu maombi yao, wakamhimidi BWANA wala hakuna miongoni mwao aliyejitwalia utukufu. Utukufu wote anampa Mungu, kwamba MUNGU wa mbinguni ndiye afunuaye siri. Danieli. 2:28,29 Danieli anasema akiwa mbele ya Nebukadneza, “lakini yuko Mungu mbinguni afunuaye siri, naye amemjulisha mfalme Nebukadneza mambo yatakayokuwa siku za mwisho…… njozi ile ilihisu mambo ambayo yangetokea siku za mwisho, tumezoea kusikia historia iliyopita lakini hapa tunaona historia ya mambo yajayo ikiwekwa wazi kwa mfalme; “Wewe, Ee mfalme, mawazo yako yaliingia moyoni mwako kitandani pako ya mambo yatakayokuwa halafu; na yeye afunuaye siri amekujulisha mambo yatakayokuwa.” Ndoto ile ya mfalme ilihusu mambo ambayo yatakuwa siku za mwisho, mambo yatakayokuwa siku za usoni kuanzia kipindi kile cha mfalme Nebukadneza hadi mwisho wa dunia(wa historia ya dunia) ndiyo yalifunuliwa katikandoto ile.
Danieli akielezea ndoto ya mfalme mbele yake anasema, Danieli. 2:31-35
“Wewe, Ee mfalme, uliona na tazama, sanamu kubwa sana. Sanamu hii iliyokuwa kubwa sana, na mwangaza wake mwingi sana, ilisimama mbele yako; na umbo lake lilikuwa lenye kutisha. Na sanamu hii kichwa chake kilikuwa ni cha dhahabu safi; kifua chake na mikono yake ni ya fedha; tumbo lake na viuno vyake ni vya shaba; miguu yake ni ya chuma; na nyayo za miguu yake nusu ya chuma na nusu ya udongo. Nawe ukatazama hata jiwe likachongwa bila kazi ya mikono, nalo jiwe likaipiga sanamu miguu yake, iliyakuwa ya chuma na udongo, likaivunja vipande vipande. Ndipo kile chuma, na ule udongo, na ile shaba, na ile fedha, na ile dhahabu, vilivunjwa vipande vipande pamoja vikawa kama makapi ya viwanja vyakupepetea wakati wa hari; upepo ukavipeperusha hata pasionekane mahali pake; na lile jiwe lililoipiga hiyo sanamu likawa milima mikubwa, likaijaza dunia yote”.
Ni hakika mfalme alishangaa kuisikia ndoto ileile aliyoiota na kuisahau.  MUNGU wa mbinguni alimfunulia Nebukadneza ndoto yake kupitia kwa Danieli, naye mfalme akakaa vema ili asikie tafsiri yake. Ndoto hii ilipotolewa kwa Danieli katika njozi ilikuwa pamoja na tafsiri yake, Mungu hakutuacha tukisie au tubahatishe tafsiri yake. Hapa tunatakiwa kuiacha biblia pekee ili itafsiri ndoto ya mfalme; Danieli. 2:36, Danieli anasema, “Hii ndiyo ile ndoto, nasi tutahubiri tafsiri yake mbele ya mfalme.” Kama vile Danieli alivyoihubiri tafsiri ya ndoto mbele ya mfalme miaka 2600 iliyopita nami naihubiri kwako hivi leo.
Kichwa cha dhahabu katika ile sanamu ilikuwa ni ufalme wa Babeli, ufalme wa Nebukadneza. Danieli. 2:37-38, “Wewe, Ee mfalme, u mfalme wa wafalme, na Mungu wa mbinguni amekupa ufalme, na uwezo, na nguvu na utukufu; na kila mahali wakaapo wanadamu, wanyama wa kondeni na ndege wa angani amewatia mikononi mwako, naye amekumilikisha juu ya hao wote; wewe u kichwa kile cha dhahabu.” Ufalme wa Babeli ulikuwa na nguvu sana za kiuchumi, kivita na maendeleo na ndiyo maana hapa unafananishwa na ‘kichwa cha dhahabu’. Ufalme wa Babeli ulitawala Dunia kuanzia mwaka 605 K.K hadi mwaka 539 K.K.
Danieli. 2:39, “Na baada ya zamani zako utainuka ufalme mwingine mdogo kuliko wewe; na ufalme mwingine wa tatu wa shaba, utakaoitawala dunia yote.” Ni kweli kabisa ufalme mdogo kuliko ule wa Babeli, yaani ufalme wa Umedi na Uajemi ulifatia baada ya Babeli nao ukatawala tangu mwaka 539 K.K hadi mwaka 331 K.K. Na baada ufalme wa Umedi na Uajemi, ufalme wa Uyunani ulifatia, na kutawala dunia nzima tangu mwaka 331 K.K hadi mwaka 168 K.K, ukiongozwa na Alexander mkuu.
Danieli. 2:40, “Na ufalme wa nne utakuwa na nguvu mfano wa chuma; kwa maana chuma huvunja vitu vyote na kuvishinda; na kama chuma kisetavyo vitu hivi vyote, ndivyo utakavyovunja-vunja na kuseta” ufalme huu wenye nguvu mfano wa chuma ni ufalme wa Rumi, rumi ya kiserikali ‘Roman Empire’ uliotawala kwa nguvu tangu mwaka 168 K.K hadi mwaka 476 B.K. Ufalme huu ulikuwa na nguvu sana nao ulienea kwa kasi, ukiangusha falme zingine. Ulitawala eneo kubwa sana ukilinganisha na falme zingine zilizotangulia, pia ufalme huu ulitawala muda mrefu kuliko falme zingine kabla yake, na katika ufalme huu Yesu mwana wa Mungu alizaliwa, akakua, akasulubiwa, akafa kifo cha aibu na kasha akafufuka kutoka katika wafu. Hivyo ufalme Rumi ya kipagani ikafananishwa na nguvu za chuma.
Danieli. 2:41, “Na kama vile ulivyoziona hizo nyayo za miguu na vidole vyake, kuwa nusu udongo mfinyanzi, na nusu chuma, ufalme ule utakuwa ufalme uliogawanyika; likini ndani yake zitakuwako nguvu za chuma, kama vile ulivyoona kile chuma kimechanganyikana udongo wa matope.”  Baada ya ufalme wa Rumi kuanguka mwaka 476 B.K haukutokea tena ufalme mmoja ulioshikamana kama falme zilizotangulia, bali ulitokea falme zilizogawanyika. Unabii wa Biblia unasema ufalme wa Rumi utagawanyika na ndivyo ilivyokuwa. Baada ya kuanguka ufalme wa Rumi uligawanyika katika falme ndogondogo kumi kamili kama ilivyokuwa jumla ya hesabu ya vidole vya sanamu ile ambavyo vilikuwa vya chuma na udongo. Na katika falme hizo ndogondogo kumi, kumekuwa na falme zenye nguvu na zisizo na nguvu. Neno la Mungu linasema, Danieli. 2:42 “Na kama vidole vya zile nyayo vilikuwa nusu chuma na nusu udongo, kadhalika ufalme ule utakuwa nusu yake una nguvu, na nusu yake umevunjika.”  Falme hizo kumi ni Alemani(Ujerumani), Franks(Ufaransa), Burgundians(Uswisi), Suevi(Ureno), Anglo-Saxons (Uingereza), Visigoths (Hispania), Lombards(Italia), Vandali, Heruli na Ostrogothi na katika falme hizi zipo zenye nguvu na zisizo na nguvu kama unabii wa Biblia unavyosema.
Danieli. 2:43, “Na kama vile ulivyokiona kile chuma kimechanganyika na udongo wa matope, watajichanganya nafsi zao kwa mbegu za wanadamu; lakini hawatashikamana, kama vile vile chuma kisivyoshikamana na udongo”. Unabii hapa unasema, ufalme uliogawanyika utafanya jitihada za kuunganika kuwa ufalme mmoja kama falme zilizotangulia ila itashindikana maana chuma hakiunganiki na udongo kamwe. Ni kweli kabisa katika historia hadi leo tunaona jitihada zikifanyika kuziunganisha falme hizi kumi bila mafanikio. Charles V, wa Uingereza alijaribu kuunganisha katika mapinduzi ya Uingereza mwaka 1648 lakini alishindwa, naye Louis XIV katika mapinduzi ya ufaransa mwaka 1789-1795, alijaribu kuiunganisha ulaya ila akashindwa kwa kuwa neno la Mungu limesema ‘Hawatashikamana’.
Jitihada hizi tunaona zinaendelea kipindi cha Napoleon katika vita yake katika bahari ya ulaya, akayashinda mataifa mengi sana ya ulaya na baadhi wakaogopa wakajua sasa wanakwenda kuungana chini ya Napoleon ila ilishindikana baada ya mipango ya Napoleon kugonga mwamba kwa Waingereza. Na kaizer Wheilm wa Ujerumani alijaribu kuunganisha falme hizi kwa vita na matokeo yake ikawa vita ya kwanza ya dunia na falme hazikuungana maana Neno la Mungu ni kweli na amini. League Of Nations ikaundwa baada ya vita ya kwanza ya dunia pamoja na kusaini mkataba maarufu wa Versaile ufaransa chini ya Charmagne waziri mkuu wa ufaransa ila hakukuwa na mafanikio yoyote bali kukazaliwa udikteta Italia chini ya Munsolin na Ujerumani udikteta chini ya Adolf Hitler wa chama cha Nazi. Hitler naye akajaribu kuziunganisha falme hizi ziwe chini ya imaya yake kwa njia ya vita, akaonekana kwa jinsi alivyoshinda falme zingine, ulaya ingeunganishwa ila jitihada zake zote zikazaa vita ya pili ya Dunia kama unabii ulivyosema.
Ukomunisti wa urusi nao ukaenea kwa kasi ulaya baada ya mapinduzi ya urusi mwanzoni mwa karne ya 20, chini ya Lenin wa chama cha Bolshevic. Mataifa mengi yakaanza sera za kikomunisti hadi hofu ikatanda kuwa ulaya inaunganishwa ila hawakushikamana kama neno la Mungu lilivyosema. Vita baridi baina ya Urusi na Marekani iliuwa ukomunisti mwishoni mwa karne ya 20, na nchi hizi zikawa katika ubepari wa mataifa ya magharibi.
Kwa sasa tunaona jitihada za kuunganisha falme hizi zinaendelea kupitia Umoja Wa Nchi Za Ulaya ‘European Union’ na Umoja wa Mataifa ‘United Nations’, na tunaona wameendelea sana hadi kuwa na sarafu moja ya ulaya ikiwa ni hatua mhimu kuelekea muungano. Ila nikwambie tu, kama neno la Mungu linavyosema HAWATASHIKAMANA ndivyo itakavyokuwa. Hata ukiangalia kuna vitisho vingi vya muunganiko huo, kwanza mdororo wa uchumi unaoikumba ulaya sasa, baadhi ya nchi kama ujerumani kukataa kutumia sarafu ya ‘euro’, nchi kuzongwa na madeni makubwa kama Urusi na Ireland, migomo na maandamano yanayoendelea haya yote ni dalili tu ulaya haitaunganika kama usemavyo unabii wa biblia.
Katika unabii, kizazi chetu tupo katika nyayo zenye chuma na udongo za sanamu ile aliyoiota mfalme Nebukadneza. Historia inaonesha tumesafiri kutoka kwenye kichwa cha Dhahabu hadi katika miguu ya chuma na leo tunaziona falme hizi zilizogawanyika kutoka katika ufalme wa Rumi, na jinsi zinavyoangaika kuungana kupitia mikataba mbalimbali lakini hazitaungana. Na ni katika siku za ufalme uliogawanyika ambapo ufalme wa Mungu utasimamishwa nao hautapita utatawala milele na milele. Danieli. 2:44, “Na katika siku za wafalme hao Mungu wa mbinguni atausimamisha ufalme ambao hautaangamizwa milele, wala watu wengine hawataachiwa enzi yake; bali utavunja falme hizi zote vipande vipande na kuziharibu, nao utasimama milele na milele.” Ufalme huu ni ufalme wa Mungu chini ya Yesu Kristo. Bablia inaweka jambo hili bayana kuwa jiwe humwakilisha Yesu Kristo, 1 Korintho. 10:4 “wote wakanywa kinywaji kilekile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafwata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo” soma pia Luka. 20:17,18 na Isaya. 28:16.
Rafiki tunaishi katika mwisho wa historia ya dunia, na hivi karibuni Yesu atakuja. Je, tumejiandaaje kumpokea? Je, Yesu akija leo atakukuta katika hali gani? Je, utaokolewa au utaangamia katika tanuru liwakalo moto? Panga kumkubali Yesu katika maisha yako leo. Hivi karibuni ufalme wa Mungu unaowakilishwa na jiwe lisilofanywa kwa mikono ya mwanadamu utaanza.
Danieli. 2:45, “Na kama vile ulivyoona yakuwa jiwe lililochongwa mlimani bila kazi ya mikono, na ya kuwa lilivunja-vunja kile chuma, na ile shaba na ule udongo,na ile fedha, na ile dhahabu; Basi Mungu aliye mkuu amemjulisha mfalme mambo yatakayokuwa baadaye; na ndoto hii ni ya hakika, na tafsiri yake ni thabiti” ni hakika kama tulivyochunguza Unabii huu wa ajabu, tumegundua kuwa ndoto ni ya hakika na tafsiri yake ilivyo thabiti kama Mungu alivyoitoa.
Katika ndoto hii ya kihistoria tumeona unabii wa biblia jinsi ulivyotimia kama Neno la Mungu lilivyosema. Historia inaonesha ukamilifu na usahihi wa Neno la Mungu kupitia unabii huu, hivyo tunapata sababu ya msingi ya kumwamini Mungu na Neno lake takatifu. Maana mambo haya yaliyotabiriwa karne 26 zilizopita tumeyeona yakitimia kwa usahihi wake. Pia hata mambo ambayo tunatazamia yatokee hivi karibuni yatatokea kwa usahihi kama tulivyoona haya mengine yakitimia na kutokea.
Jedwali No.1
ISHARA
FUNGU LINALOFAFANUA
MAANA YA ISHARA HIYO
1. Madini katika Dan. 2, Dhahabu, Fedha, Shaba na Chuma.
Danieli 2:37-40
Falme nne zilizotawala dunia yote tangu kipindi cha Danieli hadi kipindi cha ufalme wa Rumi.
2. Kichwa cha dhahabu
Danieli 2:37,38
Ufalme wa Babeli-605 K.K
3. Nyayo za chuma na udongo

Danieli 2:41
Ufalme uliogawanyika kutoka Rumi ya kipagani-476 B.K
4. Jiwe lililochongwa bila kazi ya mikono
Danieli 2:44,45; Luka 20:17,18; 1 Korintho 10:4
Ufalme wa Yesu
5. Kifua na mikono ya fedha
Danieli 2:39a
Ufalme wa pili wa Umedi na Uajemi-539 K.K
6. Tumbo na viuno vya shaba
Danieli 2:39b
Ufalme wa tatu wa Uyunani-331 K.K
7. Miguu ya chuma
Danieli 2:40
Ufalme wanne wa Rumi ya kipagani-168 K.K
Ufafanuzi wa ishara zilizotumika katika Danieli 2.


[1] Tazama kiambatanisho A
[2] Kiambatanisho B